15.04.2013 - 12:21
Dibaji
Watu wa Katalunya, katika kipindi cha historia yao, wameonesha hamu yao ya pamoja ya kujitawala wenyewe kwa njia ya demokrasia, kwa lengo la kuendeleza maendeleo yao, masilahi yao, na kutoa fursa sawa kwa raia wote, wakati huohuo wakiimarisha utamaduni wao na utambulisho wao wa pamoja.
Serikali ya kujitawala wenyewe ya Katalunya ilianzishwa kutokana na historia ya haki za Wakatalani, taasisi zao za zamani, na mapokeo ya sheria ya Katalani. Mfumo wa Bunge la Katalunya una mizizi yake, mnamo Zama za Kati, katika mabaraza ya kupitisha Amani na Suluhu na Korti ya Kaunti (ya wenye hadhi).
Katika karne ya 14 Diputació General, au Generalitat kama ilivyokuwa ikijulikana, iliundwa, na ikaendelea kujipatia uhuru wa kujitawala kwa viwango vikubwa mpaka ikawa, katika karne za 16 na 17, Serikali ya Katalunya inayoongozwa na Mwana wa Mfalme. Kwa kuanguka Barcelona mwaka 1714, wakati wa Vita vya Mirathi vya Kihispania, Philip V alipitisha Dikrii ya Nueva Planta ya kupiga marufuku haki za Wakatalani na asasi za serikali ya kujitawala wenyewe.
Tajiriba hii ya kihistoria imeshirikisha watu katika baadhi ya meneo mengine ya kiutawala, ukweli ambao uliwahusisha kwenye usuli mmoja kilugha, kiutamaduni, kijamii na kiuchumi, kwa nia ya kuimarisha na kueneza utambuzi wa kuridhiana wao kwa wao.
Katika karne nzima ya 20 hamu ya kuwa na serikali ya kujitawala ilikuwa jambo la kawaida kwa Wakatalani. Kuanzishwa kwa Mancomunitat ya Wakatalani mwaka 1914 kulikuwa hatua ya kwanza ya kufufua na kurudisha serikali ya kujitawala wenyewe, lakini ilipigwa marufuku wakati wa udikteta wa Primo de Rivera. Mwaka 1931, wakati wa kutangazwa kwa Jamhuri ya Pili ya Uhispania, serikali ya Kikatalani iliasisiwa kwa jina la Generalitat ya Katalunya na ikajaaliwa kuwa na Sheria ya Kujitawala.
Generalitat hiyo ilipigwa marufuku tena mwaka 1939 na Jenerali Franco, ambaye alianzisha udikteta uliodumu hadi 1975. Udikteta huo ulipingwa vikali na wananchi wa Katalani na Serikali ya Katalunya. Moja ya tukio muhimu la pambano la kutafuta uhuru lilikuwa kuanzishwa mwaka 1971 kwa Bunge la Katalunya, kabla ya uanzishaji tena wa Generalitat, kwa misingi ya muda, hadi rais wake kurudi kutoka uhamishoni mwaka 1977. Katika kipindi hicho cha mpito wa demokrasia, na katika muktadha wa mfumo mpya wa mikoa wa kujitawala wenyewe kama inavyoelezwa na Katiba ya Uhispania ya 1978, Wakatalani walipitisha kwa njia ya kura ya maoni ya 1979, Sheria ya Kujitawala ya Kikatalani, na katika mwaka 1980 uchaguzi wa kwanza wa Bunge la Katalunya ulifanyika.
Katika miaka michache iliyopita, pamoja na uimarishaji wa demokrasia, wingi wa nguvu za kisiasa na kijamii za Kikatalani zimesukuma kupatikana kwa mageuzi ya miundo ya kimahakama na kisiasa. Jitihada ya hivi karibuni, ilikuwa mchakato wa kugeuza Sheria ya Kujitawala ya Kikatalani iliyoanzishwa na Bunge mwaka 2005. Matatizo na vikwazo vilivyowekwa na taasisi za Serikali ya Uhispania, hasa hukumu ya 31/2010 ya Mahakama Kuu, ilikuwa kinyume kabisa na mabadiliko ya kidemokrasia yaliyotokana na matakwa ya pamoja ya watu wa Katalunya, na yaliyosababisha msingi wa serikali kutoendelea kujitawala, jambo ambalo leo linajidhihirisha lenyewe katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na siasa, mamlaka ya kisheria, fedha, jamii, utamaduni na lugha.
Watu wa Katalani, kwa kutumia njia mbalimbali, wameeleza dhamira yao ya pamoja kushinda hujuma zilizowekwa na Serikali ya Uhispania. Maandamano makubwa ya Julai 10, 2010, chini ya kaulimbiu ‘Sisi ni Taifa’, na ya Septemba 11, 2012, chini ya kaulimbiu ‘Katalunya, Dola Mpya ya Ulaya’, ni matamko dhidi ya kukataliwa kwa maamuzi ya watu wa Katalani.
Fauka ya tarehe 27 Septemba, 2012, na kwa mujibu wa Azimio 742/IX, Bunge la Katalunya linaasisi haja ya watu wa Katalunya kujiamulia kwa njia huru na ya kidemokrasia, mustakabali wao wa pamoja kupitia kura ya maoni. Dhamira hii ilikuwa wazi na iliamuliwa waziwazi kutokana na uchaguzi wa mwisho wa Bunge la Katalunya uliofanyika Novemba 25, 2012.
Ili kufanikisha mchakato huu, Bunge la Katalunya, lilipokaa katika kikao cha kwanza cha Bunge la 10, na kwa mujibu wa matakwa ya raia wa Katalunya yaliyotolewa kwa njia ya demokrasia wakati wa uchaguzi uliopita, lilipitisha yafuatayo:
Azimio la Uhuru na la Haki ya Kuamua kwa Taifa la Katalani
Kwa mujibu wa dhamira ya demokrasia ya wengi wa watu wa Katalani, Bunge la Katalunya huanzisha mchakato wa kuleta na kuendeleza haki za raia wa Katalunya ili kuamua kwa pamoja mustakabali wao wa kisiasa, kuambatana na kanuni zifuatazo:
-Uhuru. Watu wa Katalani wana, kwa sababu ya uhalali wa kidemokrasia, uhuru wa kisiasa na kisheria.
-Uhalali wa Kidemokrasia. Mchakato wa kutekeleza haki ya kuamua itakuwa ya demokrasia ya hali ya juu, hasa kwa kuhakikisha hiari mbalimbali na ambazo zote
zitaheshimiwa, na, kwa kujadiliana na kuzungumza kati ya wanajamii wa Katalani. Lengo litakuwa kwamba, tangazo litakalofuata baada ya majadiliano litaonesha dhamira ya watu wengi, na ambalo litakuwa dhamana ya kimsingi ya haki ya kuamua.
-Uwazi. Zana zote muhimu zitawezeshwa ili idadi ya watu wote na jamii yote ya Wakatalani wapate habari kamili na maarifa kuhusu mchakato wa haki ya kuamua, na kuendeleza ushiriki wao katika mchakato huo.
-Dayalojia. Nchi ya Katalunya itaanzisha na kushiriki katika mazungumzo na mashauri au mapatano na Serikali ya Uhispania, taasisi za Ulaya na mashirika ya kimataifa.
-Mshikamano wa kijamii. Mshikamano wa kijamii na kieneo wa Katalunya utahakikishwa, na hivyo hivyo hamu yao, kama itakavyopendekezwa katika matukio mbalimbali na jamii ya Wakatalani, ili kudumisha taifa moja.
-Mfumo wa Ulaya. Kanuni za waanzilishi wa Umoja wa Ulaya zitalindwa na kuendelezwa, hasa haki za msingi za raia wake, demokrasia, kujitolea kwa ajili ya ustawi wa taifa, kushirikiana na mataifa mbalimbali ya Ulaya, na kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
-Sheria. Miundo ya Sheria zote zilizopo zitatumika kuimarisha demokrasia na kutekeleza haki ya kuamua.
-Jukumu Kuu la Bunge. Bunge la Katalunya, likiwa taasisi inayowakilisha watu wa Katalunya, lina jukumu kubwa la kuongozea mchakato huu, na kwa hivyo, itakuwa muhimu kuamua na kubainisha taratibu na mienendo ya mchakato ambayo itahakikisha kanuni hii.
-Ushiriki. Bunge la Katalunya na Serikali ya Generalitat wawe washiriki wa mstari wa mbele katika ngazi ya mitaa, kwa kuwa na idadi kubwa ya nguvu za siasa (kupitia vyama), katika mambo muhimu ya kiuchumi na kijamii, katika mashirika ya kiutamaduni na kiraia ya nchi yetu, na kubainisha taratibu zitakazohakikisha kanuni hii.
Bunge la Katalunya linahimiza raia wote kujihusisha sana katika mchakato wa kidemokrasia kwa ajili ya haki ya kuamua ya Wakatalani.
Nyumba ya Bunge, Januari 22, 2013